Friday, November 03, 2006

Wag

 
Jina la kejeli ‘wag’ lilipewa kijana mmoja tulikuwa tunasoma na yeye shule ya Msingi.Jina lenyewe likawa lamfaa kabisa.Kijana huyu aliketi karibu nami tulipokuwa darasa la nane.Tulikuwa marafiki sana.Wag aliweza kuchekeshwa na mambo ambayo wengi wanaweza kupita tu bila kutilia maanani sana.Kama wakati wadudu walioitwa Nairobi fly walipoivamia shelu yetu.Lo!Hizo zilikuwa siku za shaka.Mvua ya – el nino –ilikuwa ikinyesha wakati wadudu wale walipojitokeza.Walifanana na bendera ya inchi ya Kenya kwa rangi zao za kijani,nyeusi na nyekundu,walijaa kila kona ya shule.Si kwa nyasi,kuta,juu vizingitini,vitandani,kote.

Ikawa kana kwamba wakamwagwa na adui.Wanafunzi walijawa na hofu .Huyu mdudu alikuwa na umajimaji uliomtoka mwilini,na uliposhikana na ngozi ya mwanaadamu uliichoma ikawa mfano wa aliyemwagiwa maji moto.Baadaye ngozi ingeanza kuchanika na kuanguka.Nyuma ikiacha ngozi ngumu nyeusi na uchungu mwingi.Wasichana wa darasa letu walipatwa na huyu mdudu.Ilibidi waketi mchana kutwa kwenye bweni,huku wapangusa machozi. Kuyaacha yatiririkie juu ya vidonda vilivyo achwa nyusoni zao kungekuwa kama kujinyonga kwa kamba.Uchungu wa kifo.
Bweni ilikuwa kama wadi ya wagonjwa.Wavulana kadhaa walipatwa pia lakini walijikaza kufika darasani.Wag alikuwa na shida sana.Shida ya kujaribu kujizuia kuangua kicheko-wanakaa kama wamejifunga maski nyeusi-alininong’onezea.Nakumbuka tulicheka.
Hadi ile siku Nairobi fly Mmoja jasiri alitembelea pua la wag.Chali alivimba pua na macho ikafikiana.Halafu akawa abadilika rangi kama kinyonga.Wag hakukanyanga darasani kwa muda.Aibu labda,lakini ngozi yake ilipochanika na kuanguka,hakubaki na weusi,badala yake alibadilika akawa mzungu.
Sikucheka.
Wag alijicheka akakosa pumzi.

Mwalimu wa Kiingereza alipenda kuuliza maana ya majina tofauti..Jioni moja wakati nwa prep tulikuwa tunafanya marudio ya mtihani wa kejeli-mock-
Wag akajibu swali,kueleza maana ya white collar jobs.Mojawapo ya aina zingine za kazi zilizokuwa zimetajwa katika mpangilio wa majibu ya kuchagua ilikuwa-blue collar jobs.Niliinua mkono kuelezea maana.Nikasema ni zile kazi nje ya ofisi.Waweza kuamini mwalimu alipandwa na hasira karibu anitukane?
‘Najua nyinyi wawili mnapenda mchezo sana!Wewe wag huo ulaghai wako utakoma leo!’Alidhani tulikuwa tunamchezea tu,kwa sababu tulikaa pamoja na mara nyingi tuliambiana majibu.Baada ya kufunza kidogo alisema tukamngojee kwa ofisi.
Kwa kumsihi sana nilifaulu kumshawishi kuwa wag hakuhusika kamwe na jibu langu,na kuwa niliamini elezo langu lilikuwa shwari.
Alituamini.
Nafikiri san asana ni kwa vile wag alikuwa amenyamaza kimya hata tabasamu halimtoki.
Siku hizi nimekuja kujua kuwa kunazo blue collar jobs,na hata pink collar.Pengine katika darasa la nane,silabasi haikuruhusu kujua aina zingine,mwanafunzi wa 8-4-4 asichanganyikiwe.
18-10-06

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home